SERIKALI IMEENDELEA KUSUKUMA MAGEUZI SEKTA YA ELIMU

JamiiVoice
By -
0

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali imeendelea kusukuma mageuzi ya sekta ya elimu kwa kasi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa vipaumbele vya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya siku 100 tangu aapishwe.

Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni, Prof. Mkenda amesema dhamira ya Rais Samia ni kujenga mifumo imara itakayoboresha ujifunzaji na kuwaandaa wanafunzi kumudu ujuzi unaohitajika katika ajira na uchumi wa kisasa.

Prof. Mkenda ameeleza kuwa Serikali imetekeleza hatua muhimu mbili katika kuimarisha ubora wa elimu nchini.

Hatua ya kwanza ni uandaaji na uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali na wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili. Mpango huo ulizinduliwa tarehe 29 Januari 2026 jijini Dar es Salaam na Rais Samia, na unalenga kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayefika darasa la tatu bila kumudu stadi hizo za msingi.

Hatua ya pili ni uzinduzi wa mpango wa pamoja kati ya waajiri, vyuo vya ufundi stadi na vyuo vikuu, uliofanywa tarehe 9 Februari 2026 na Makamu wa Rais, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi jijini Dar es Salaam. 

Mpango huo unakusudia kuimarisha uhusiano kati ya mfumo wa elimu na soko la ajira, kuongeza mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi na kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa.


Prof. Mkenda amesema Serikali inatarajia mpango huo kupunguza changamoto ya kukosekana kwa uwiano kati ya ujuzi wanaopata wahitimu na mahitaji ya soko la ajira (skills mismatch), sambamba na kupanua fursa za mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo mbalimbali nchini.

Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default