Bungeni:
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027 wizara yake itajielekeza kutekeleza vipaumbele vitano muhimu vinavyolenga kuimarisha ubora wa elimu na kukuza matumizi ya sayansi na teknolojia nchini.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo bungeni, Prof. Mkenda amesema kipaumbele cha kwanza ni kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, kufanyia mapitio sheria zinazohusu sekta ya elimu, pamoja na kuandaa miongozo na kutoa mafunzo mbalimbali kwa watendaji na wadau wa elimu.
Kipaumbele cha pili ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo vya amali ili kuwajengea vijana ujuzi wa ufundi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Amesema kipaumbele cha tatu kitahusisha kuongeza fursa na kuboresha elimu ya awali, msingi, sekondari na mafunzo ya ualimu, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuinua kiwango cha ufundishaji na ujifunzaji nchini.
Kipaumbele cha nne ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu kupitia maboresho ya vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ili kuandaa wataalam wenye uwezo na ushindani wa kimataifa.
Aidha, amesema kipaumbele cha tano ni kuimarisha uwezo wa nchi katika utafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwa lengo la kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda.
