
Na Mwandishi Wetu - DAR ES SALAAM
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, ameitaka TTCL kuandaa vifurushi vya Faiba Mlangoni Kwako vinavyokidhi uwezo wa familia, wanafunzi, vijana na wafanyabiashara wadogo na wa kati.
Waziri Kairuki ametoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa Awamu ya Pili ya huduma hiyo jijini Dar es Salaam, akisema upanuzi wa mtandao wa faiba unapaswa kwenda sambamba na uwezo wa wananchi kumudu huduma.

Amesema Mradi wa Faiba Mlangoni Kwako unapaswa kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali yakiwemo makazi yanayokua, masoko, maeneo ya biashara, viwanda, shule, vyuo, vituo vya afya na ofisi za Serikali Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha, ameagiza TTCL kuhakikisha huduma inakuwa ya uhakika na malalamiko ya wateja yanashughulikiwa kwa wakati.

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, CPA Moremi Marwa, amesema Shirika linalenga kuongeza zaidi ya Home Pass 400,000 katika Awamu ya Pili.
Amesema TTCL imejenga zaidi ya 280,000 Home Pass katika Awamu ya Kwanza na kutumia teknolojia ya GPON katika kuendeleza huduma ya nyuzi za macho.
Kwa mujibu wa Waziri, gharama nafuu na ubora wa huduma ni msingi wa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu ya kidijitali unawafikia wananchi wengi na kuchochea shughuli za kiuchumi.








